Tuesday, 19 September 2017

NDUGU WAGOMBANAPO MGENI HURITHI MALI YAO



Na San Andy

Paris Ufaransa

Juzi lilitokea tukio la kushangaza kidogo ni pale Neymar Jr na Edinson Cavani walipo gombea kupiga penalty iliyopatikana katikati ya mchezo, Sishangai sana tukio lile kutokea kati ya Cavani na Neymar kwakua kwa kiasi kikubwa wana maisha yanayo fanana. Hili limenikumbushia wahenga wangu Didier Drogba na Frank Lampard kugombania penati kwenye mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Wigan

Tofauti na sintofahamu ya Lampard na Drogba nadhan wao walikuwa na mtazamo tofauti. Droga alitaka ufungaji bora ila lampard aliwazia zaid ubingwa. Kwa hawa wengine ni tofauti kidogo. Cavani ameishi nyuma ya kivuli cha Zlatan Ibrahimovic kwa misimu kadhaa pale Park De Princess, Cavani ameishi akiamini hakuna mchawi wa muda lazima jioni itafika jua litachwea na yeye atang'aa




Wakati Cavani anawaza haya kule Camp Nou Neymar anachoka kufanya kazi ya mshumaa kuteketea ili Messi apate mwanga katika kuelekea kwenye njia yake ya mafanikio. Anacho amua kufanya ni kuondoka hapo kwenda kuanzisha utawala wake sehemu nyingine. Neymar aliamini ndizi imeshakomaa na alihitaji zaidi pesa kuliko ndizi mbivu hivyo aliamua kupeleka mkungu wote Kule Paris kwa gharama ya Euro milion 222.

Nakumbuka Mrisho mpoto kwenye wimbo wake wa njoo uchukue alisema "Watu wakikimbia wanapozika huangukia kwenye maiti nyama" Pale PSG Cavani anaamini huo ndio wakati wake na yeye kuwa na utawala wake hii ni maiti nyama bado hatujawaza kuizika. Kule Barca Neymar kakimbia mazishi akiamini mazishi yana mchelewesha kwenda kutawazwa kama mfame mpya wa Barca kaja kuangukia PSG kwenye maiti nyama




Cavani na Neymar wote wana ndoto ya kuwa wachezaji bora pale PSG na dunia kwa ujumla. Ulimwengu huu ili uwe mchezaji bora lazima ufunge magoli mengi ndio maana unawaona vijana wale wakigombea kupiga penati.

Katika wimbo uleule wa Mpoto anasema "Ukitaka kujua mwendo wa mjinga mpe kilemba uone" Mchezaji ghali zaidi duniani hiki ni kilemba kichwani kwa Neymar kwakua amekivaa anataka kubadili mwendo na kutembea kama kilemba kinavyoitwa. Anahitaji kuonyesha kuwa yeye kweli ni ghali ili aonyeshe hayo inabidi afanye zaidi ya wenzake hapa ndipo sisi watazamaji tunaona mwendo wa mjinga.

Mfalme wa PSG hiki kilemba kipo mikononi mwa Cavani anahitaji kuvaa kichwani, ili kilemba kikae kichwani lazima afanye kama Ronaldo pale Real Madrid au Messi pale Barcelona. Kuwa kama wale lazima yeye afanye zaidi ya wengine pale Paris Saint German.

Mpira wa miguu ni tofauti sana na michezo kama mbio za magari (Formula One) pikipiki na Tennis katika michezo hii huitaji uwepo wa mtu mwingine ni wewe pekee ndie unaamua hatma yako uwe bora au usiwe bora

Katika mpira ubora wa kila mchezaji unategemea team work. Lazima uwe na mahusiano mazuri na wenzako ili ubora wao ukusaidie wewe kuwa bora wafanye wajiskie furaha kuwa mshumaa wako. Messi na Ronaldo wamefanikiwa kuwafanya Suarez na Benzema wajiskie furaha kuwaka ili wao waone njia na kuendelea mbele katika safari zao,Kitu cha muhimu ni kuheshimiana

Waungwana husema "Wakisimama nyuma yako walinde,Wakisimama pembeni yako waheshimu ila wakisimama dhidi yako wapige" Cavani na Neymar hawataki kusimama pamoja ili kila mmoja awe pembeni ya mwenzie heshima ichukue nafasi. Kila mmoja anaona mwenzie ni kikwazo cha yeye kufikia ndoto zake kila mmoja anamuona mwenzie ni mtu aliyesimama dhidi yake ni wa kupigwa tu. Wanasahau kuwa wakisimama pamoja kwa kuheshimiana wata wapiga watao simama dhidi yao ambao ni kina Hazard, Dybala, Dembele, Messi na Ronaldo

Hawa ni ndugu wanaoishi sehemu moja kupigana wao kwa wao kunampa jirani nafasi ya kurithi mali yao. Kama wataendelea kugombea penati ule uchezaji bora wa dunia ambao ingeweza kuwa mali yao majirani watarithi. Nilichokiona kwa Mobeto na Diamond huenda basi mmoja wao kati yao (Neymar na Cavan) watakuja mpaka clouds kutupa ubuyu. Kwaheri

Imeandikwa na San Andy
Imeandaliwa na Privaldinho


No comments:

Post a Comment