MAYWEATHER NA PACQUIAO TENA?
Na Priva ABIUD
Mbwa siku zote anakula kwa uwezo wa kasi yake, nguvu yake na pumzi yake. Mara nyingi mbwa hata asipokuwa na akili ataishi vizuri tu na atanenepa vyema.
Mourinho na Klopp wanakutana tena. Wote ni makocha wanaotegemea mapafu na kasi za wachezaji wake kupata mafanikio. Tofauti yao ni kwamba mmoja anapigana ngumi za hela (mourinho) na klopp anapigana ngumi za kitoto
Mourinho akipigana huwa anafunika uso (kujilinda zaidi) kama mabondia wa ngumi za kulipwa wanavyofanya (mfano Mayweather) lakini Klopp yeye anaamini zaidi ushapu wake wa ngumi za haraka haraka bila kujilinda kama tulivyokuwa tukipigana utotoni bila kujali kama kacha tumbo na uso wazi.
Mchezo wa klopp na Mourinho, huwa unaboa sana. Mmoja anakuwa anajilinda na kumvizia mwenzake. Mwingine yeye anaamini kuwa kushambulia kwa kasi ndiko kutamfanya mbwa wake ampate digidigi wake kiurahisi.
Mourinho amekuwa na matokeo mabovu sana kwa klopp licha ya ngumi zake za kulipwa. Akiwa na Madrid mwaka 2012 ( Borussia 2 1 Madrid) (Real Madrid 2 2 Borussia Dotmund ) 2013 ( Borussia 4 1 Madrid) ( Real Madrid 2 0 Borussia) akiwa na chelsea (chelsea 1 3 liverpool) akiwa na Man Utd wametoka droo michezo miwili. Hivyo Mourinho ameshinda mchezo mmoja tu dhidi ya klopp huku akipoteza mitatu na kudroo mitatu pia.
Mchezo huu utaboa sana kama bado Mourinho ataendelea na mbinu zake za kimayweather. Ataondoa ile ladha ya ushindani wa liverpool na Man utd. Mfumo wa kukimbia kimbia ulingoni ili kutafuta point angalau moja unaondoa ladha.
Mfumo wa gegeni wa kushambulia sana wa klopp utamfanya Mourinho ajilinde sana . Lakini kwa mawazo yangu mimi sioni kama kuna sababu hiyo. Man Utd ina washambuliaji wazuri zaidi na wenye kasi na akili kuzidi hata wa liverpool au sawa na liverpool ( Coutinho, Mane, Firmino na Salah) huku Man utd ( Mikhitaryan, Martial, Lukaku na Mata) wote hawa wana uwezo unaolingana na wanapaswa wapigane kiume.
Kiungo cha katikati cha Man utd naona ni bora sana, (Matic, Herrera, na Carrick) liverpool wana Emre, Henderson, Wijnaldum) kiungo cha liverpool bila unafiki sio cha kuifanya United irudi kuzuia Uso.
Beki la Liverpool ndo kabisa sitaki kuizungumzia maana sio vyema kumzungumzia marehemu vibaya.
Man utd msimu huu imefunga magoli 22 na kuruhusu magoli mawili tu, liverpool imefunga magoli 13 na kufungwa 12) ila Man utd haijacheza mechi kubwa ukilinganisha na liverpool
Kwa takwimu Man utd Wanaenda Anfield wakiwa kama timu kubwa, ila kwenye kichwa Mouringo yeye anakwenda na Mawazo ya kumaliza round ya 12 bila kupigwa KO ilimradi tu apate pointi kadhaa iwe 1 au 3.
Mchezo wa Mayweather na Manny Pac uliboa sana. Hata michezo ya Man utd na liverpool msimu uliopita ulikuwa mbovu. Na nina hakika hata huu wa jumapili kwa namna Mourinho ninavyomjua kwenye akili haendi kushindana ila anakwenda anfield kuzuia goli lake. Kila kheri
Leave a Comment