nifikiriavyo


BRAZUCA YA DAMU CHANGA NA MATARAJIO MAKUBWA YA MASHABIKI.
Macho na masikio ya wapenda soka ulimwengu kote yameelekezwa kule Rio de Janeiro nchini Brazil, kule ambako mpira umetuama, kule ambako mpira ni kama dini kule ambako kuanzia nyumbani, mtaani, barabarani lugha ni moja tu nayo ni mpira wa soka. Wakati flani Roberto Carlos aliulizwa “Selecao” wanapocheza inamaana gani kwa wananchi wa Brazil, bila kung’ata maneno alijibu “Kila Brazili inapocheza popote ulimwenguni kwa muda wa dakika 90 watu wanasahau matatizo yao kwasababu kila mwananchi anaacha shughuli zote na kufwatilia mechi”
Lakini taarifa zaidi zinasema Brazili inapocheza hasa wakati wa kombe la dunia kuanzia wauza karanga njiani mpaka wafanyakazi wa serikali huchukua muda kuangalia mechi kwenye luninga ama kusikiliza redioni, pia wafanyakazi serikalini na makampuni binafsi hutoka masaa matatu chini ya muda wa kawaida ili tu kupata wasaa wa kujiandaa kuishangilia timu ya taifa lao. Hiyo ndiyo nchi ambayo kuanzia tarehe 12 Juni 2014 kombe la dunia litaanza kwa timu mbalimbali kutafuta alama 3 muhimu.
Wakati Wabrazili wakilisubiri kwa hamu Kombe la dunia kuanza nyumbani, kwingineko ulimwenguni majina matatu ya wachezaji mahiri dunia hayaachwi kutamkwa, kwenye vijiwe vya kahawa, sehemu za kucheza drafti, vibanda na bar mbalimbali zinazoonyesha mpira, Christiano Ronaldo, Lionel Messi na Neymar ndiyo majina matatu maarufu midomoni mwa wapenzi wa soka, wachezaji hawa wanasuburiwa kuona nani atamfunika mwenzake uwanjani.
Lakini wakati wapenzi wa soka wakibaki na Ronaldo, Messi na Neymar midomoni, huu ni mwaka wa kombe la dunia ambao vipaji vingine vingi vinasuburiwa kuwika, kama ilivyokuwa kwa Pele pale Sweden 1958, Franz Beckenbauer pale England 1966, Michael Owen pale Ufaransa 1998 na Thomas Muller pale Korea ya kusini na Japani 2002 ndivyo tunasubiri tuone nani atawika pale Brazili baada ya wengi wao kuwika kwenye ligi zao za nyumbani na hasa kwenye michuano ya mabingwa wa Ulaya.
Katika listi hiyo ya wachezaji vijana kabisa wanaosubiriwa kuwika kuna kipa Thibaut Courtois kutoka Ubelgiji kwa kila aliyekuwa anaifwatilia timu ya Atlectico Madrid msimu huu aliona ubora wa kipa huyu ktk umri mdogo tu wa miaka 22, halafu kuna beki Raphael Varane ktk umri wa miaka 21 ni kama unamwangalia Lilian Thuram alipokuwa kwenye ubora wake pale Ufaransa, halafu kuna Eden Hazard kutoka Ubelgiji, nafikiri baada ya Ronaldo, Messi na Neymar anafwatia Hazard kusubiriwa kwa hamu na wapenda soka ulimwenguni.
Ufaransa kuna Paul Pogba ktk umri wa miaka 21 ni kama anatembea kwenye nyayo za Zidane pale “les bleus” ana nguvu na skills za kufanya sehemu ya katikati ya uwanja ya Ufaransa ipendeze, halafu kuna kiungo mshambuliaji James Rodriguez miaka 22 toka Colombia anatumia mguu wa kushoto ambao unachagizwa na jezi yake namba 10, kutokuwepo kwa Falcao ni kama kusema kazi kubwa atakuwa nayo Rodriguez anayekipiga pale Monaco.
Nyumbani Brazili kuna kijana Oscar Dos Santos huyu anachukuliwa kama Kaka mpya kwenye kikosi cha Selecao akiwa na miaka 22 tayari ameweza kuuonyesha ulimwengu wa soka ubora wake akikipiga ktk timu ya Chelsea.
Pia kuna kiungo toka Schalke 04 Julian Draxler akiwa na miaka 20 anatarajiwa kuwa chachu ya mafanikio ya Wajerumani pale Brazili na kwa kuumia kwa Reus basi tutegemee mengi toka kwa Draxler ikitegemea kama atapewa muda mrefu uwanjani, nyumbani kwa Malkia Elizabeth Uingereza kuna Rose Burkley akiwa na miaka 20 amekuwa na msimu bora kabisa pale Everton, ni mchezaji anayeweza kukupa goli ama pasi ya goli kutokana na kuwa na miguu yenye kasi na makini, halafu kuna na Alex Oxlade-Chamberlain(20) na Raheem Sterling(19) ambao wote hawa ni aina ya wachezaji ambao wanampa kiburi kocha wa Uingereza Roy Hudgson ktk eneo la ushambuliaji hasa kwa mipira ya “counter attack”.
Hivyo ni baadhi tu ya vipaji vinavyosubiriwa kuwika kwenye fainali za kombe la Dunia lakini pia makocha na mawakala wa vilabu mbalimbali duniani wakiwa tayari kuwapa mikataba minono. Listi ni ndefu ila wachezaji hawa wachache wanakupa picha ya kombe la Dunia la 2014 kujawa na wachezaji wenye umri mdogo na mahiri.
Nafikiri tukijiandaa kuelekea Rio pale Brazili tujikumbushe na kujifunza kupitia nukuu hii ya Pele wakati alipohojiwa na mtandao wa FIFA.Com alisema,

“I was born to play football, just like Beethoven was born to write music and Michelangelo was born to paint” akimaanisha “nilizaliwa kucheza mpira, kama Beethoven alivyozaliwa kuandika muziki na Michelangelo alivyozaliwa kupaka rangi” wewe shabiki wa soka popote ulipo jiulize we ulizaliwa kufanya nini hapa duniani?
NAWASILISHA
@Cico cicod

No comments

Powered by Blogger.