Ukitupa makombo umkumbuke na ibramovic

MAKALA:

KILA UNAPOTUPA CHAKULA MKUMBUKE IBRAHIMOVIC.

Labda nianze kuuliza maswali machache kabla
sijaendelea kuandika makal haya, nani amewahi kumwaga mabaki ya chakula nyumbani? nani
amewahi kuagiza chakula hotelini ama kwa Mama
Ntilie na kula nusu tu ya chakula hicho na kuacha
kingine kimwagwe ama kupewa mbwa? Namini
tupo wengi sana katika hili.
Lakini mshambuliaji wa PSG na timu ya taifa ya
Sweden Zlatan Ibrahimovic ametumia sehemu ya
mwili wake kutukumbusha kwamba wakati
tunatupa chakula ama kuwapa mbwa mabaki ya
vyakula vyetu kuna watu milioni 805 ambao
wanateseka kwa njaa duniani kote.

Ibrahimovic baada ya kufunga magoli mawili
kwenye mchezo wa ligi kuu nchini Ufaransa dhidi
ya Caen Jumamosi iliyopita alivua jezi yake ya juu
na kuonyesha “tattoo” ya majina 50 ya watu
mbalimbali ambao wanateseka kwa njaa duniani
ikiwa ni njia ya kuunga mkono mpango wa chakula
duniani kutoka Umoja wa Mataifa (WFP).
Majina kama Carmen, Mariko, Antoine, Lida,
Rahma na Yaae yamechorwa kwenye mwili wa
Ibrahimovic hii inamaanisha popote duniani
utakapomkumbuka na kumshangilia mshambuliaji
huyu pia utaweza kuwakumbuka wahanga milioni
805 wa njaa duniani.

Nyuma ya ya “tattoo” za majina haya 50 kuna
sauti za watoto, wazee, vijana, kinamama
wajawazito, walemavu ambao hakuna
anayewafahamu wala kuwakumbuka na hata
kutaka kujua hali zao ingawa wengine inawezekana
ni ndugu, jamaa, majirani na hata marafiki lakini ni
vigumu kuchukua hatua kutaka kuwasaidia.

Inawezekana ikawa ni ngumu kuwasaidia watu
wote milioni 805 ambao wanakufa kwa njaa
duniani kote lakini kwa vile vitu ambavyo
tumejaliwa na Mungu hebu tuonyeshe kujali,
kwamba wakati wewe unatupa kipande cha mkate
jalalani kumbuka kuna mtu alikunywa chai bila
kitafunwa wakati huo huo ama wakati unamwaga
wali karibu sahani nzima jalalani kumbuka kuna
mtu mchana ulipita bila ya kuweka kitu mdomoni.

Hebu tujiulize kuna umaana gani kwenda hotelini
na kuagiza chakula ambacho labda kinauzwa
shilingi 5000 halafu ule kidogo na kutupa sehemu
kubwa ya chakula hicho huku ukikumbuka kabisa
kuna watoto wa mitaani kadha wa kadha ulikutana
nao njiani ukielekea hotelini ambao walikuomba
hela ya chakula na ukawaambia kwa hasira “sina
hela na msinisumbue”.

Hebu leo na sisi tuwe wajasiri sio kwa kuchora
“tattoo” kama Ibrahimovic bali wakati tunapoenda
kula hotelini, migahawani, kwa Mama ntilie ama
nyumbani tunaweza tukamchukua mtoto mmoja
wa mtaani ama hata jirani na kushiriki nae chakula
hicho ili kuepuka kukitupa bila sababu za msingi
huku tukiwaacha wengine wakifa kwa njaa.

Tukumbuke msemo unaosema kwamba “swala sio
ulikuja vipi duniani bali swala ni uliiacha vipi dunia
baada ya kuondoka (kufa) “ hivyo tujue kwamba
wakati mwingine hatuhitaji kuwa milionea kama
Bakhresa ama Mengi ndipo tuweze kutoa msaada
kwa wenzetu, katika huo huo udogo wetu mambo
makubwa yanaweza kutimia na tukaweza kuifanya
dunia ibaki kuwa sehemu bora ya kuishi.

NAWASILISHA. Cico cicod @arusha

No comments

Powered by Blogger.