KUNA MWENYE SWALI TENA KWA MECK MEXIME?
Na Oscar Oscar
Tumekuwa na makocha wengi wazawa ambao kwa sasa wamegeuka kuwa wapiga kelele tu. Hawana timu wanazofundisha isipokuwa kazi yao kubwa imebakia kukosoa wenzao na kuponda wachezaji kwa kigezo cha taaluma yao. Mexime ameendelea kujipambanua na Makocha wapiga kelele, alianza hivyo akiwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro na sasa anafanya kazi iliyotukuka akiwa na Kagera Sugar ya mkoani Kagera. Kuna mwenye swali tena kwa Meck Mexime? Nadhani hakuna.
Tanzania tumekuwa na makocha wengi wenye vyeti lakini hawana timu. Kazi yao ni kukaa kijiweni na kuanza kufanya uchambuzi! Kikubwa kutoka kwao ni kujisifia kuwa na vyeti vingi. Kuwa na watu wengi wenye vyeti wakati hawana timu, hakulisaidii Taifa letu. Meck anapaswa kutumiwa na wengi kama mfano wa Kuigwa. Kwanza si mjivuni na amejitenga kabisa na unazi wa Simba na Yanga hali ambayo makocha wengi wazawa hawana. Pamoja na kuukosa Ubingwa wa Ligi kuu Tanzania Bara msimu huu lakini kitendo cha kuoongoza Kagera Sugar akiwa ndani ya msimu wake wa kwanza hakipaswi kuchukuliwa pouwa.
Kwa kigezo cha msimamo wa Ligi Kuu Tanzania iliyomalizika wiki iliyopita, Mecky Mexime ndiyo kocha bora Mzawa na pengine ni mtu anayestahili kushinda kabisa hata tuzo ya kocha bora wa Msimu. Yaani kwa hili siwashbiri Bodi ya Ligi wanitajie kocha bora wa msimu wakati mimi mwenyewe nimeshuhudia upambanaji na mafanikio ya Mexime msimu huu. Mecky anawakumbusha makocha wetu wazawa kwamba ni muda wa kutoka kijiweni na kutafuta timu kuanzia msimu ujao.
Kozi mbalimbali zinazotolewa za makocha zitakuwa hazina maana kama tutaendelea kuongeza idadi ya watu wenye vyeti wakati hawana timu wanazofundisha. Kazi aliyoifanya kocha Mecky Mexime kama angekuwa kocha wa Kigeni, kuna uwezekano mkubwa Simba, Yanga na Azam fc huenda wangeshaanza kumuwinda kwa ajili ya kumalizana nae kuelekea maandalizi ya msimu ujao. Ni kama alivyokuwa Mtibwa Sugar, kikosi chake kinauiano sahihi wa vijana na wachezaji wenye uzoefu.
Mecky kaiongoza Mkubwa Sugar kushinda mechi 15, sare nane huku akipoteza michezo saba tu. Namba hazidanganyi, Mecky anastahili kuwa kocha bora wa msimu wa 2016/2017. Joseph Omog, kocha wa Simba na George Lwandamina wa Yanga wamefanya vizuri kuliko Mecky lakini ukitazama Ukitazama ubora wa vikosi vya timu hizo ukilinganisha ni kile cha Kagera Sugar, utakubaliana na mimi kwamba Mecky amepambana zaidi kuifikisha timu yake hapo ilipo kiliko hao wengine wa juu.
Kocha Omog anakosa sifa kwa sababu tu ya kuukosa Ubingwa na Lwandamina pia kumbuka ameichukuwa timu katikati ya msimu baada ya Yanga kuachana na kocha wao Hans Van Der Pluijm. Tunahitaji makocha wengi wazawa wapambanaji kama Mecky Mexime ili walete ushindani kwa hawa makocha wa Kigeni badala ya kukaa vijiweni na kuponda uwezo wa makocha wa kigeni wanaoendelea kushinda mataji kila kukicha.
Mchanganyiko wa kina Juma Kasseja na Mbaraka Yusuph, bila shaka umelipa chini ya Mecky Mexime. Sijawahi kumuona Mecky akihofia mchezaji wake kuchukuliwa na timu nyingine, amekuwa pia Bingwa wa kuendeleza vipaji vya vijana wa Kutanzania na kutumia pia uzoefu wa wachezaji wakongwe baada ya kutupiwa virago na timu za Simba na Yanga. Kama Mecky angekuwa kwenye timu yenye bajeti kubwa ya usajili na yenye kutoa huduma bora kwa wachezaji msimu mzima, kuna uwezekano mkubwa angeweza kumaliza juu ya Simba na Yanga. Mecky sio kocha wa kawaida, anapaswa kutazamwa kwa jicho lingine. Kwa hili sisubiri Bodi ya Ligi initangazie Kocha bora, Mexime anatosha msimu huu. Huyu ni kioo cha makocha wazawa msimu huu.
Amemfanya Mbaraka Yusuph kuwa moto kweli kweli, mabao 12 aliyofunga msimu huu yatakuwa yanawatoa udenda sana Simba na Yanga. Mecky pia amemfanya Kasseja arejeshe heshima yake kwa kuonyesha kiwango bora kabisa msimu huu na hasa pale alipokutana na timu zake za zamani, Simba na Yanga. Bado kuna mtu anaswali tena kwa Mecky Mexime? Mimi sina hata moja, kwa kumaliza nafasi ya tatu akiwa na Kagera Sugar anastahili kuwa kocha bora wa msimu.

Leave a Comment