SARAKASI ZA RUSHWA KWENYE SOKA LETU "SAMAKI MKUNJE, ANGALI MBICHI
Mwinchande, kst (Mtalimbo)
Habari za jumamosi wana jamvi wenzangu, hongereni kwa kufikisha mwezi wa saba wengine mkiwa bado mpo Dar maana si kwa mkwala ule wa Mkulu.
Leo nalitandika jamvi langu kwenye baraza nadhifu ya jengo maridadi kabisa lenye roshani kadhaa zilizonakishiwa kwa vioo vya rangi ya samawati inayovutia kuliangalia hususani nyakati za mawio na machweo ya jua. Kwa juu limeandikwa kwa maandishi yenye ujazo "TAASISI YA KUPAMBANA NA RUSHWA".
Mahala hapa ni pazuri sana kwa mazungumzo yetu ya leo naomba msiogope sogeeni karibu, hao Askari walioshika mitutu hawana tatizo na sisi wana kazi maalum ya kuwadhibiti wala rushwa wakifika mahali hapa.
Wiki hii tumeshuhudia tufani kali ikiikumba tasnia ya soka letu, jaka moyo limetukumba baada ya kushuhudia viongozi wa ngazi ya juu kabisa wa TFF pamoja na klabu ya Simba wakikamatwa na hatimaye kufikishwa mahakamani na Taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa TAKUKURU kwa madai ya kujihusisha na vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya ofisi kubwa zaidi ni ule msamiati unaowachanganya watu wengi unaoitwa "Utakasishaji wa pesa"
Leo sitozungumzia kadhia hiyo iliyowapata wakina Bwana Malinzi raisi wa TFF na katibu mkuu wake Bwana Mwesigwa pamoja na Bwana Avena raisi wa Simba na makamo wake Bwana Kaburu kwa kuwa kesi yao ipo Mahakamani na sheria hairuhusu kuingilia uhuru wa Mahakama.
Nitajikita zaidi kuzungumzia juu ya tabia na mwenendo tuliojijengea wa kulindana na kuleana kwenye vitendo viovu kama vile tabia ya kula rushwa au matumizi mabaya ya ofisi. "Majuto ni mjukuu" leo tunawalilia akina Malinzi lakini tumesahau kuwa tulishindwa kumkunja samaki angali mbichi.
Tumeshindwa kumkunja Samaki akiwa mbichi leo amekwisha kauka sasa amevunjika tunaanza kulialia na kuwalaumu watu tuliowaacha wakakauka na kushindwa kukunjika.
Tatizo la matumizi mabaya ya ofisi kwenye mfumo wetu wa soka limekuwa ni la siku nyingi sana. Pale TFF kuna habari zilivuma kuhusu ukabila lakini lilibaki kuwa ni minong'ono tu hakuna aliyekuwa tayari kumfunga paka kengele kulikunja kabla halijakauka na hatimaye kuvunjika. Pia vitendo vya rushwa vilikuwa vinavuma mithili ya pepo za kusi lakini tulivifumbia macho, leo samaki amekwisha kauka tunaanza kulaumiana.
Tulishuhudia vitendo vya rushwa iliyodhahiri wakati wa chaguzi za kuchagua viongozi wa mikoa. Lakini tulinyamaza kimya na kuishia kupiga porojo vijeweni na kwenye magroup ya whatsapp, hatukuwa tayari kumkunja samaki angali akiwa mbichi sasa leo maji yamezidi unga tuiache Takukuru ifanye kazi yake.
Tulishuhudia vitendo vya upangaji wa matokeo kwenye ligi zetu hususani ligi kuu na ligi daraja la kwanza. Kamati za TFF pamoja na viongozi waandamizi walishutumiwa kupewa rushwa ili wapindishe kanuni na kuwapa haki wasiostahili kupata haki. Tuliliacha hili tatizo bila kulikunja likiwa bichi tukabaki kuzungumza kwenye vijiwe vya kahawa tu, sasa leo limekwisha kauka tuwaache Takukuru walikunje wao.
Tulishuhudia malalamiko ya kila siku kuhusu rushwa ilivyojipenyeza kwenye mikataba inayoingia TFF na kampuni mbalimbali. Kuna mikataba ina utata kwenye mambo ya zabuni lakini tulifumbia macho hatukuwa tayari kumkunja samaki angali mbichi, leo wadau wengi wa soka wanaonekana kuvurugwa ni hii skendo kama ni habari mpya kwao. Ngoja tuwaache Takukuru watusaidie kumkunja samaki aliyekauka maana sisi tumeshindwa kumkunja akiwa mbichi.
Tulishuhudia tuhuma nyingi za marefa wetu kuhusu kupokea rushwa ili watumike kuwapa matokeo ya ushindi timu fulani lakini tulizidharau na kuona ni uzushi kwa kuwa kuna bahadhi ya timu walinufaika na mpango huo. Tulishindwa kumkunja samaki akiwa mbichi sasa leo tuwaache wanaojua kumkunja samaki aliyekauka wafanye kazi yao.
Tulishuhudia ubabaishaji katika makusanyo na matumizi ya michango ya pesa kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka. Tulinyamazia taarifa za vijana wa Serengeti boys kupujwa mgao wa fedha zao, tulishindwa kumkunja samaki akiwa mbichi sasa leo naomba tuendelee kunyamaza ili Takukuru wawakunje samaki waliokauka.
Kwa upande wa timu ya Simba tulishuhudia kauli na vilio vya baadhi ya wachezaji kuhusu kuchezewa kwa mikataba yao lakini hakuna aliyewasikiliza na kuna baadhi ya mashabiki waliwatetea viongozi wao. Pia tulishuhudia utata kwenye mchakato wa mauzo ya baadhi ya wachezaji mfano wake ni mauzo ya Samata na Okwi lakini tulifumbia macho hatukuwa tayari kumkunja samaki akiwa mbichi, sasa na leo pia tuendelee kufumbia macho ili wenye uwezo wa kufumbulia macho waweze kumkunja samaki aliyekauka.
Wanajamvi wenzangu nawashukuru sana kwa usikivu wenu kwenye mada yetu ya leo. Naomba sasa mnyanyuke ili niweze kulikunja jamvi letu maana wenyewe wanataka kufungua ofisi zao waanze kazi kwani kwa mbaaali naona kuna watu wengine wanaletwa mmoja kama amevaa likofia likubwa na wengine naona kama wanasare za rangi ya njano na kijani.........
"Samaki mkunje, angali mbichi" pia waswahili wanasema "Kila zama na nabii wake" pia tusisahau "Mwenda tezi na omo, marejeo ngamani"
Leave a Comment