JASHO LA SCOTT PARKER, NA UFALME WA AKINA LAMPARD NA GERRARD
Na Privaldinho
Mpira wa kiingereza ni mgumu sana. kwanza ni mgumu kwa aina ya uchezaji na ni mgumu kwa mchezaji kufanikiwa na kuimbwa. kuna mtu kama Lee Barry cattamole, akiwa na umri mdogo kabisa wa miaka 19 tu na siku 47 alikuwa nahodha ya klabu ya Middlesborough lakini nani anayemjali sana wakati yupo timu inayoshabikiwa na mji tu?
Unapokuwa unaangalia mpira wa kiingereza utamu wake ni vurugu vurugu za akina Roy Keane, viatu vya akina barry, makelele ya akina Steven Gerrad, Hasira za akina Wayne Rooney, uchokozi wa akina Joe Barton na mashuti ya akina Frank Lampard.
Dimba la katikati la Engand limewapoteza akina Lampard na Gerrard, tumebakiwa na Michael Carrick tu. Scott Parker nae ameondoka na Jasho lake.
Licha ya watu wengi kumsema vibaya kuwa hakuwa na kipaji lakini amefanya mambo makubwa. Huyu ndiye aliyekuwa mchezaji bora wa mwaka wa Chalton Athletic Mwaka 2002 akiwa na miaka 21 tu, 2003 alitwaa tuzo ya mchezaji bora chipukizi wa ligi kuu wa mwaka. mchezaji bora wa West Ham mwaka 2009, 2010, na 2011. Pia waandishi wa habari walimpa tuzo ya mchezaji bora mwaka 2011 kwa kusakata kabumbu vyema, mwaka huo huo alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa England, kisha akaingia kwenye orodha ya wachezaji 11 bora wa mwaka.
Mbali na mafanikio hayo bado ameondoka na jasho lake hakuna aliyemrushia hata sabuni ya jamaa. Ndio amestaafu. Kwa miaka kadhaa huyu amekuwa akitajwa kama Viungo wa katikati bora kabisa kutoka England. Tunaweza kusema huyu ni Kiungo wa pili mchezeshaji pia mkabaji. Walio wengi wameshindwa kutofautisha kati ya kiungo mkabaji na Holding midfielder. Holding midfielder kwa lugha nyingine ni kiungo mshughulikaji. Holding Midfider sio namba 6 kama tunavyodhan, huyu ni mtu anayeunganisha timu (Pirlo, Scholes), anayezuia timu pinzani (Daren Fletcher, Ander Herrera), na anayepumzisha timu yake (Michael Carrick, Basquet Sergio) pia wapo wenye jichoa la tatu wanaweza kuona alipo nama 9 kama Toni Kroos, Xavi na wale waendeshaji (kukokota) kama Jackie Wilshere. kiujumla ni viungo ambao wapo free sana uwanjani na hawana jukumu moja licha ya kwamba wanakaa dimba la katikati tu.
Huyu ndiye aliyempa Modric uhuru wa kutawala dimba la juu kwa amani. Sura ya Parker ilijificha kwenye maumbile ya akina Sergio Basquet, Marehemu Cheik Tiote, Alexandra Song, Carrick na Steven Gerrard. Hao walionekana kwa sababu timu zao zilikuwa na mashabiki wengi na zilipata mafanikio ambayo yaliwapa heshima kubwa. Ni aina ya kiungo ambaye sio lazima acheze rafu nyingi. kama unakumbuka Simon Kuper aliwahi kumsifia sana Paulo Maldin kuwa ni beki ambaye alikuwa anacheza Takolin moja (kutelezea miguu kwa lengo la kukaba) moja kila baada ya mechi mbili lakini bado alihesabika beki bora duniani.
Kwa miaka ijayo sijajua nani atavaa viatu vya Scott Parker hata vya Carrick ukiachilia mbali Gerrard, timu ya taifa ya England Namwona Eric Dier tu. Paul Merson amemwimba sana Dier, binafsi namwona Dier amekaa kiukabaji zaid. Parker hajaimbwa sana wakati anaondoka ila itafika wakati watakosa kiungo kama yeye na kisha wataanza kuzalisha viungo ambao media zitampa sifa ambazo hana. Nilichobatika kukiona kwa Parker ni kile kile ambacho Gerrard aliwapa wana Liverpool, tofauti walikuwa mazingira tofauti. Sina lengo la kumshusha Gerrad, ila kumbuka mtoto aliyezaliwa kwenye mali ni rahisi sana kujua kufanikiwa kuliko wa umasaini. Gerrard na Lampard walicheza klabu kubwa na walifanya makubwa, Parker alicheza mavumbin ndio maana hakuokota dhahabu. Ni wachezaji wa daraja sawa, tatizo nyota yake ilikuwa nyeusi. Watu wa Liverpool wanaweza kuona kama namtukana Gerrad . Hapana. Hebu tuwaangalie kwenye majukumu matatu tuone bila kuangalia mafanikio kitimu

1. kiungo wa kati (kuchezesha timu) takwimu zao kwa ujumla Parker amecheza michezo 368 Gerrard amecheza mechi 504.
Parker amepiga pasi 10,490 (Pasi 28 kwa kila mchezo) huku Gerrad akiwa amepiga pasi 15, 108 (pasi 29 kwa kila mechi) Gerrad amempita Scott pasi zaidi ya 5000 lakini ikumbukwe Gerrad amecheza michezo mingi zaidi kuliko Parker (michezo 200) (kimahesabu maana yake 200x wastani wa pasi 28 kwa kila mechi za Scott tunapata pasi 5600 maana yake Scott kimahesabu alipaswa kuwa na pasi zaidi ya 16,000 kama angecheza michezo 200 aliyozidiwa.

2. kusaidia timu katikati na kupandisha mashambulizi (Mipira mirefu Gerrard mara 1,500, Parker 689, Gerrad alitengeneza nafasi 34, Huku Parker akitengeneza 13. Parker pasi mpitisho 130 Gerrard 195, Gerrard ametengeneza magoli 92 Parker 21. kimahesabu Gerrard ameibuka mshindi kutokana na ndiyo nafasi aliyocheza zaid uwanjani.

3. Ukabaji (Manowari/kutelezea/takoling) Scott Parker amecheza mara 882 huku Gerrard mara 579. Parker ameharibu pasi za Maadui mara 486, Gerard mara 356. kuondoa hatari Gerrard Mara 435 Scott mara 331. Parker amenyang'anya mpira maadu mara 1324 huku Gerrard (1330), mipira ya juu Parker ameokoa mara 1422, Gerrard 1271. hapa wamekingiana kifua licha ya Parker kumzidi kwa kuwa yeye alikuwa kiungo wa pili mkabaji.

kwa takwimu hizo kwenye akili yako kumbuka licha ya kupishana takwimu kwa karibu sana, lakini Idadi ya mechi wamepishana mno. kwa mechi hizo chache Parker alizocheza bado hajapitwa sana kwa takwimu na Gerrard. Sijamshusha Gerrad hata kidogo. nimemtumia Gerard kwa sababu ndiye kiungo wa Kiingereza mwenye akili zake na uwezo mkubwa anayeweza kuzurura dimba la chini mara chache na akafanya yake. Gerrard atabaki kuwa legend na shujaa wa Anfield lakini hainizuii kusema sijaona kiungo wa kiingereza anayechafua dimba la kati kama Parker (samahan usimjumuishe Carrick). Eric Dier Kazianayo. Sipendi sana kumzungumzia Michael Carrick kwakua ni kiungo wa kipekee ambaye kwa Man utd kuziba pengo lake sio kazi rahisi. Carrick ndiye kiungo bora kabisa wa katikati kwa miaka 10 iliyopita ndani ya England kwangu . Ni aina ya viungo wa kihispaniola huenda anakaribia pasi 20,000 huko. Na Gerrard atabaki kuwa kiungo wa Dimba la juu bora kabisa kwa waingereza yeye na Lampard. Wala sina haja ya kuwazungumzia. Kwaheri Parker
Leave a Comment