WAKATI HEKALU LINA TEKETEA, ISCO ANZA KUJI INIUA

Na San Andy

Tarehe 21 July 356 BC hii ni tarehe muhimu sana katika historia ya dunia, Usiku wa siku hii mjini Ephesus lililokuwa jengo zuri zaidi duniani lilikuwa likifutika katika uso wa dunia kutokana na moto uliowashwa na Herostratus kwaajili ya kupata umaarufu, Wakati jengo hili linateketea usiku huo huo katika mji wa Pella alikuwa ana zaliwa Alexander The Great mmoja kati ya watawala wenye historia kubwa katika uso wa dunia hii

Kuteketea kwa uzuri na umaarufu wa hekalu la Artemis kulitoa nafasi ya kuinuka kwa  Alexander. Pale jijini Madrid ndani ya Santiago Bernabeu historia mpya ya soka inategemewa kuandikwa, Ni kwasababu  Francisco Roman Alarcon Suarez "ISCO" anategemewa kuongeza mkataba wake na Real Madrid hadi mwaka 2022


Kinachotokea Real Madrid ni sawa  na kilichotokea Uturuki mwaka 356 BC, Real Madrid hakuna hekalu la Artemis ila kuna Cristiano Ronaldo huyu ndio kitu kizuri zaidi machoni mwa Madridista, Huyu ndie mchezaji bora duniani mbele ya macho yao licha ya kuwa huwa wanamzomea ila hii haibadili ukweli wa mioyo yao kuwa Artemis yao ni Ronaldo, Wana jivunia vingi sana ila kwasasa huyu ndo sababu inayo wafanya watembee vifua mbele.


Mfalme Alexandra The great

Kule Uturuki Herostratus alichoma moto hekalu lile ili na yeye akumbukwe kwenye historia ya dunia, Bahati nzuri iliyopo Real Madrid ni kuwa kinacho teketeza hekalu lao sio moto bali ni umri, Moto uliteketeza hekalu kwa usiku mmoja tu ila umri una mteketeza Ronaldo taratibu sana kwahiyo wanaohitaji kupata umaarufu baada ya kupotea kwake wanapaswa kuanza kuinuka taratibu kama Alivyofanya Alexander The Great


Adolf Hitler aliwahi kusema "Ili ufanikiwe unapaswa kuzaliwa wakati sahihi" Ndani ya Bernabeu namuona Isco kwanza amezaliwa wakati sahihi sana tofauti na kaka zake Xavi & Iniesta waliozaliwa wakati wa Messi na Ronaldo. Isco yupo kwenye kizazi cha kina Hazard, Neymar, Dybala hawa wote ni wachezaji wazuri katika kipindi chao kila mmoja anaweza kuacha historia katika ulimwengu maana wachezaji wengi wa kizazi chake wana fanana kitu kimoja "Lack of Consistency" ubora wa kudumu kwa kipindj kirefu. Ni wachezaji wanaotegemea mechi na mechi.


Wengi wao msimu huu wakifanya vizuri msimu unaofuta wanafanya vibaya hii inatoa nafasi kwa wengine kufanya vizuri kwenye club zao na dunia kwa ujumla. Jambo zuri jingine kwa upande wa Isco ni kuwa mpira kwasasa upo kwenye falsafa za Dikteta Hitler aliwahi kusema "Nguvu haiangaliwi kwenye kuzuia bali katika kushambulia" kwa takribani miaka kumi hivi sasa mchezaji bora wa dunia kwa mwaka amekuwa anatokea katika nafasi ya ushambuliaji kama ni kiungo ni kuanzia wale wanao husiana na ushambuliaji, Mtazamo wa dunia kwasasa mchezaji bora ni yule anayefunga magoli mengi


Tayari amefanikiwa kuanzisha utawala wake katika timu ya taifa ya Hispania. Naongea hivi bila shaka yoyote kuwa ukitaja timu ya taifa ya Hispania huwezi kuacha kumtaja Isco. Hispania bila Isco ni harusi bila pilau.


Isco yupo kwenye klabu bora yenye wachezaji bora ambao watamsaidia sana kuacha historia katika soka la dunia. Ila Isco na Hazard wana kitu kimoja ambacho naona kita wachelewesha au kita wanyima kabisa fursa ya kupata wasaa wa majina yao kutajwa kama washindi wa tuzo ya mchezaji bora wa dunia tuyaache haya labda watabadilika


Wakati hekalu la Artemis linateketea Alexander alikuwa anazaliwa,wakati Raul Gonzalez ana teketea Cristiano Ronaldo aliinuka. Umri nao unaelekea kuteketeza umri Messi na Ronaldo taratibu sana naona huu ni wakati sahihi wa Isco kuanza kuinuka pale Madrid.


Wakati huo huo Neymar, Hazard, Pogba, Dybala, De Bruyne, Dele Alli na wengineo nao wata anza kuinuka atakaye kaza miguu yake ndie ataweza kusimama na kuonekana na akiweza kuendelea kukaza miguu tutamuona kwa muda mrefu sana kama Messi na Ronaldo. Mtoto mlafi siku zote ndiye anayeshiba kwenye sherehe. Nawakumbusha tu Isco na wenzake kwenye sherehe likishushwa sinia usiulizie kijiko we bugia matonge makubwa makubwa.


Yote tisa Isco ana kazi kubwa ya kufanya maana anainuka eneo ambalo hekalu lina dondoka ni kazi yake kufanya watu wasahau kuhusu hekalu lile na kumtazama yeye pekee. Asipokuwa makini watu wata changanya udongo na kujenga hekalu jingine huku akishuhudia. Nimweleze tu kuwa Licha ya Asensio kuonekana kibarua, akumbuke kwamba hata kibarua huegeuka fundi kwa uzoefu anaopata kwa mainjinia.

#AllTheBestIsco
#SandAndy


No comments

Powered by Blogger.